“Pasipo maono watu hushindwa kujizuia” Mithali 29:18
Maono
ni kama kesho ya mtu.Kesho
ni siku ambayo hutarajiwa na haijaonekana bayana bado, na hakuna mwanadamu
yeyote chini ya jua aijuaye kesho yake ipoje isipokuwa amejuzwa na Mungu ajuaye
mambo yote kabla hayajatukia. Kesho ni siku ambayo ni matokeo ya kile kitu
ambacho kimefanyika leo; kesho huandaliwa ndani ya leo, Mungu ndiye hutoa
jawabu kama iwe kama vile ulivyoiandaa.
Kuna
msemo wa kiingereza usemao, “Yesterday is history (jana ni historia), today is
a gift (leo ni zawadi), tomorrow is a mystery (kesho ni siri iliyofichika)” hii
inaonyesha kuwa katika maisha yote ya mwanadamu kuna siku tatu tu yaani jana,
leo na kesho na mwanadamu anapaswa kuzitumia siku zote hizo kwa faida yake
mwenyewe na kunufaisha jamii inayomzunguka pia.
Jana
ni siku ambayo imepita na hukutengenezea uzoefu (CV) ambao waweza kuwa mzuri au
mbaya, na kamwe hautoweza kurudi jana kuibadilisha jana yako ila unaweza
kuitumia Leo kuifanya kesho isijekuwa kama jana. Jenga tabia njema ya
kutojisifia kwa mazuri uliyofanya jana kwa kuwa kujisifia kutakufanya ujisahau
kuwa unapaswa kusababisha mambo makubwa kutokea tena na tena kamwe usijaribu
kujilaumu kwa vile ulivyoshindwa jana kwa kuwa itakufanya uwe muoga wa kujaribu
kufanya mambo makubwa leo. Lakini mazuri ya jana yanaweza kutumika kama marejeo
kuwa kama jana nilishinda basi na leo pia naweza kushinda kama ilivyokuwa kwa
Daudi aliporejea kuua simba na dubu pale alipotaka kupambana na Goliathi.
Kesho
ni mimba ambayo imetungwa leo na yapaswa kujifungua ni muhimu sana kuzingatia
ili kuweza kujifungua mtoto aliye mzuri na hii inatokana na mimba hiyo
imetungwaje na katika hali gani. Kujifungua mimba hii kunahitaji nguvu ya mbeba
ujauzito na pia Mungu akusaidie kujifungua salama.
Maono
huweza kuwa sawa na ahadi ambayo imetoka kwa Bwana kwa kuwa ahadi ni mambo
yatarajiwayo na hayajaonekana bayana bado, ufananaji wake unatokana na kuwa
ahadi ya Mungu huwa ni mambo ya kesho na ndiyo maana yanaitwa mambo
yatarajiwayo na hayajaonekana bado, na yakichanganywa na hakika pamoja na
bayana ambayo ndiyo imani hayabaki kuitwa maono au ahadi kwa kuwa tayari
yametimia.
Kitu chochote unachokifanya leo
kinaonesha kuwa kesho yako itakuwaje.
|
Ni lazima uione kesho yako ukiwa leo kwa kuwa kesho yako inategemea
sana na wewe unaona nini ndani yako mwenyewe ukiwa leo, na si kuona tu, pia
unakiri nini kwa kuwa kuna nguvu katika ukiri wa maneno, na si ukiri tu, bali
ni nini ukifanyacho leo kinaweza kuitimiza kesho yako. Kitu ukionacho ndani
yako, ukikiricho na hata kukifanya hugeuka kuwa tabia na kikiwa tabia mwishoni
huja katika uhalisia wa utimilifu wake.
Kesho
yako haitakuja kama muujiza yaani umeamka na kuiona tu inatimia, hapana ni
mchakato mrefu ambao unakuhitaji kutia juhudi za kutosha ili iingie kwenye
utimilifu wake. Kama haujaanza kuwaza kuwa kesho yako itakuja kuweje kamwe
usijedhania kama kitakuja kutimia kwako kitu ambacho hujawahi kukiwaza hata
siku moja, mtu anaweza kuhangaika na kitu ambacho amewahi kukiwaza hapo awali
kuliko kile kitu ambacho hajawahi kuwaza kabisa.
Kijana
mmoja alikuwa akisafiri kuelekea mahali asipopafahamu, baada ya kusafiri muda
mrefu akakuta sehemu kuna njia panda na akamuona mzee mbele yake katika hilo
eneo, akamuuliza Yule mzee nipite njia gani nifike sehemu ninayotaka kufika,
Yule mzee akamuuliza mahali anapotaka kuelekea ili amuelekeze njia ya kupita;
kijana akajibu kuwa hafahamu sehemu anayopaswa kwenda, Yule mzee akamwambia
apite njia yoyote kati ya zile azionazo au hata arudi alipotoka pengine anaweza
kufika mahali anapotaka kufika. Mfano huu ni sawa na mtu asiye na maono katika
maisha yake ni lazima awe mtu anayeshindwa kujizuia na hana muelekeo maalum.
Lazima
uione ndani yako kwanza. Mwanadamu huwa vile anavyowaza ndani yake kwa kuwa
lile wazo humpa hamasa ya kufanya kazi ili litokee na wazo pia la ndani yake
huweza kumfanya kukata tamaa ya kufika mbali. Mtu mmoja akasema kuwaza ni
kuwaza tu kama umewaza mambo makubwa au madogo ni bora ukawaza vitu vikubwa labda
waweza kuwa mtu mkubwa. Lakini kuwaza tu pasipo kuchukua hatua hakufai.
Mithali
23:7 “7 Maana aonavyo nafsini mwake,
ndivyo alivyo.” Yaani ukitangulia tu kuona kuwa wewe ni maskini mkubwa ni
lazima uwe, ni lazima ujifunze kuona vyema. Watu wakubwa duniani kabla ya kuwa
vile walivyo, walitangulia kuona ukubwa ndani yao kwanza na kisha wakaanza
kufanya kazi kwa kuwa ile picha waliyoiona ndani yao huwatesa kuifikia.
Katika
biblia neno ‘unaona nini?’ limeonekana mara saba na siku za wiki zipo saba, ina
maana ya kusema kila asubuhi BWANA huweza kukuuliza ‘unaona nini?’ mpaka
zikaisha siku saba za wiki na itakapoanza jumatatu ataanza na unaona nini? tena
mpaka Ijumaa huku akiunganisha na neno usiogope kwa kila siku uionayo katika
uwepo wako duniani.
Kofi
Anan ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa baada ya kuingia UN
katika nafasi ya kawaida tu akamwandikia mama yake ujumbe na kumtaarifu kuwa
siku moja ni lazima aje kuwa katibu wa umoja wa mataifa. Alivyoona ndivyo
ilikuja kutokea na kule kuona kwake kulimlazimu kutotulia na kuwa na juhudi
kubwa sana ili baadae aje kuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa.
Kama
kuna picha tayari unaiona ndani yako ya jinsi vile unavyopaswa kuwa ni muhimu
sana kuzingatia kuwa picha ile ni nguvu ya kukufanya upigane hata kuitimiza;
ila mbaya zaidi ni kwa mtu asiye na maono kwa kuwa hana picha ndani yake ni
vigumu kwa yeye kufanya kitu cha msingi.
Maandiko
yanasema katika Mithali 29:18 kuwa “18
Pasipo maono, watu huacha kujizuia”, tafsiri ya asili ya kiebrania maono
imetafsiriwa kama ‘hazon’ ambayo humaanisha mafunuo ya neno la Mungu, na
huendelea kwa kumaanisha kuwa pasipo neno la Mungu kufunuliwa kwa watu ni
lazima watu waende katika njia ya upotevuni. Mahali popote ambapo neno la Mungu
halijafunuliwa ni lazima watu waangamie na kuendelea katika njia zao wenyewe
kwa kuwa bado huwa kwenye mabano ya wafanye kipi na kuacha kipi.
Kwa
kuangalia maono pia mtu yeyote ambaye hajafunuliwa ni maono gani alionayo ni
kazi sana kuwa katika njia sahihi. Jamii inayotuzunguka watu wengi hukosa maono
na ndiyo maana huishia kufanya vitu vya ajabu sana. Maono ni ile picha ya ndani
aionayo mtu kwa habari ya kesho yake na kama mtu haoni picha yoyote ndani yake
ni vigumu kufanya vitu vya msingi vya kimaendeleo.
Mtu
mwenye maono hata kama anaonekana maskini kwa wakati huo ni mtu wa tofauti kwa
kuwa maono ni muongozo wa utendaji kazi wa mtu huyo na ni lazima afanye mambo
ambayo yanapelekea utimilifu wa maono hayo na huishi maisha ya kujizuia katika
mambo yoyote ambayo hayamsaidii kufikia mwisho wake. Mtu mwenye maono hawezi
kutulia hata maono yake yawe yametimia.
Maono hutoa muongozo wa jinsi mtu
apasavyo kuwa na hata jamii ya kushirikiana nayo.
|
Nikiwa sehemu fulani nahudumu baada ya huduma nikamuuliza kijana
mmoja, je! Unataka kuja kuwa nani? yule kijana akaniambia nataka kuja kuwa
dereva na alikuwa anasoma, na nilipomuuliza kwa nini anataka kuja kuwa dereva
alieleza kuwa, ni kwa sababu wazazi wake hawana uwezo wa kumuendeleza kimasomo,
nilitafakari kuwa mtu huyu anataka kuja kuwa dereva kwa sababu ya hali ngumu ya
kiuchumi, ni vizuri ila katika mazungumzo nikagundua kuwa amekata tamaa ya
kufanikiwa zaidi kwa sababu ya hali yake ila mwenye maono hata kama ana hali
ngumu kamwe hataacha kuukiri ushindi wake kuwa pamoja na ugumu uliopo ninaweza nikafika
pale ninapokusudia na hata kama nitachelewa kulingana na vikwazo vya hali
niliyonayo sasa ila nitahakikisha nimefika.
Pamoja
na kuwa mfanya kazi wa ndani kwa Potifa na kisha kupelekwa gerezani na kuwa
mfungwa, bado Yusufu aliendelea kuitazama na kuikiri ndoto yake ya kuja kuwa
mtu mkubwa, mazingira mabaya na ya kukatisha tamaa hayakumfanya Yusufu akate
tamaa na kubadilisha aina ya ndoto. Ni ukweli sana kuwa ugumu wa maisha ni
sababu kuu sana ya kusababisha watu kuyaacha maono yao ya uhalisia na kuingia
katika mengine ambayo si maono yao.
Mtu
asiye na maono ni lazima mambo yake yawe ovyo ovyo kwa kuwa hakuna mwongozo
sahihi unaoweza kumzuia asifanye yale ambayo anataka kufanya. Maono ni muongozo
kwa mtu mwenye nayo katika mambo yote na humuongoza kuwa sehemu sahihi kwa
wakati sahihi na kuwa na watu sahihi. Na ni nadra sana kumkuta mtu mwenye maono
anafanya mambo ambayo hayawezi kumsaidia kufikia utimilifu wa maono yake.
Ni muhimu sana kwa mtu kuiona kesho yake ndani
yake na aione katika uzuri ndipo anaweza kutumia muda wake vizuri kutimiza yale
ayaonayo. Kuona ni jambo jema sana ila mtu anaweza kuogopa kuwaza mambo makubwa
na hii hutokana na mtu kujidharau na kuona kuwa ana uwezo mdogo sana ndani
yake, hili ni tatizo la kiimani, kutojitambua na kujidharau; ni lazima utoke
kwenye eneo hili la kukosa kujiamini na uanze kuona kuwa unaweza.
Maono makubwa, huleta taabu kubwa,
(The greater the revelation, the greater the tribulation)
|
Wakati
fulani nikiwa na rafiki yangu Christina akanena na kuniambia kwamba “the
greater the revelation, the greater the tribulation,” akimaanisha kuwa (maono
makubwa huambatana na taabu kubwa). Ukifuatilia kwenye biblia utaona kuwa watu
wote waliobeba maono makubwa ndio watu waliopata taabu kubwa hata utimilifu wa
maono yao. Usikate tamaa unapoona majaribu yamekuwa ni makubwa sana kwa upande
wako, kaa utulie huku ukitafakari kuwa ni uzito wa maono uliyonayo ndiyo sababu
kuu ya kuteseka kwako.
Mfano
ni Mtume Yohana aliyepata maono ya kitabu cha ufunuo akiwa katikati ya mateso
makubwa na kuwekwa katika kisiwa cha Patmo na Mtume Paulo ambaye alipata mateso
makubwa kulingana na ukubwa wa maono aliyokuwa amebeba.