Ajira sio
salama tena kama ilivyokuwa zamani. Kwa sasa maisha yamekuwa ghali huku kipato
cha ajira kikiwa hakitoshelezi. Hii inawafanya waajiriwa wengi kufikiria
kuingia kwenye biashara.
Lakini pia
kuingia kwenye biashara sio rahisi kama ambavyo mtu anaweza kuona. Kuna
changamoto zake nyingi na kama ndio unatokea kwenye ajira huku ukiwa na
mahitaji makubwa ya fedha, sio rahisi kuacha ajira na kuingia kwenye biashara
moja kwa moja.
Kushindwa
kuingia kwenye biashara moja kwa moja sio mwisho wa wewe kufanya biashara.
Inawezekana kabisa ukawa na biashara huku unaendelea na kazi yako unayofanya
sasa.
Zifuatazo ni
baadhi biashara tano unazoweza kufanya wakati bado unaendelea na ajira yako.
1. Biashara ya
mtandao(network marketing).
Hii ni
biashara ambayo unaweza kuifanya kwa muda mchache kwa siku au kwa wiki na
ukaanza kujitengenezea kipato hata kama kwa sasa bado umeajiriwa. Kupitia
biashara hii wewe unakuwa msambazaji wa huduma au bidhaa kwa njia ya kuwaambia
wengine uzuri wa bidhaa au huduma zile na wanaponunua wewe unapata kamisheni.
Kuna faida nyingine nyingi kupitia biashara hii kama kuweza kutengeneza timu
kubwa na ikakuongezea kipato kikubwa.
Kama unataka
kufanya biashara ya aina hii jifunze kwanza kwa undani kwa kujisomea wewe
binafsi kisha chagua kampuni unayoweza kufanya nayo na jiunge ili uanze kujenga
biashara yako. Uzuri wa biashara hii ni kwamba kwa sehemu kubwa utafundishwa
mbinu za kuweza kuendesha biashara yoyote.
2. Kuwa mkufunzi
binafsi.
Kama kuna
ujuzi wowote ambao unao, basi jua kuna watu ambao pia wanauhitaji. Wewe unaweza
kuwa mkufunzi binafsi kwa ule ujuzi ambao unao. Kwa mfano kama wewe ni mwalimu,
basi unaweza kufanya biashara ya kuwa mwalimu binafsi kwa watoto ambao wazazi
wao wana uwezo wa kulipia gharama ya juu kidogo. Wewe unakwenda kuwafundisha
watoto hao majumbani kwao. Unatoa huduma nzuri na unahakikisha watoto wanaweza
kufaulu vizuri.
Kama unataka
kufanya biashara hii, chagua watoto wa aina gani unataka kufundisha, kisha
angalia katika watu unaowafahamu ni wangapi wenye watoto wanaoweza kufaidi
huduma zako. Tafuta wachache wa kuanza nao hata kwa gharama za chini, fanya nao
kazi vizuri na kama watafurahia waombe wazazi wao wakutambulishe kwa marafiki
zao ambao wanaweza kufaidika na huduma unayotoa.
3. Ushauri wa
kitaalamu.
Kwa kazi
yoyote ambayo unaifanya, wewe una utaalamu fulani. Utaalamu huo unaweza
kuwasaidia watu wengi sana ambao hawajui pa kuupata. Kama wewe ni daktari,
unaweza kuwa unawapa watu ushauri kuhusu afya zao, wapo wengi sana wanaohitaji
ushauri ila hawajui kama unaweza kupatikana, tena kwa bei rafiki kwao. Kama
wewe ni mwanasheria uliyeajiriwa, unaweza kuwa unatoa ushauri wa kisheria kama
biashara yako ya pembeni.
Kama unataka
kuingia kwenye biashara hii ya kutoa ushauri wa kitaalamu, jua ule utaalamu
ambao unao, kisha angalia ni watu gani wanaweza kunufaika na ushauri wako kisha
tafuta wachache wa kuanza nao. Endelea kutoa huduma hii ya ushauri ukilenga
kujenga jina na baadae unaweza kutoza gharama au kuongeza gharama kama ulianza
na kidogo.
4.
Huduma za kitaalamu.
Hii ni
tofauti na ushauri wa kitaalamu, hapa unatoa huduma kabisa. Kwa mfano kama wewe
ni mhasibu uliyeajiriwa, unaweza kuanzisha biashara yako ya pembeni ya kutoa
huduma za kihasibu kwa biashara ndogo ndogo. Wafanyabiashara wengi wadogo
hawawezi kumudu gharama kubwa za kupata huduma za uhasibu, kama wewe unaweza
kuwaandalia mahesabu yao kwa gharama ambayo wanaweza kuimudu, unaweza
kutengeneza biashara kwenye eneo hilo.
Kama wewe ni mwanasheria unaweza kutoa
huduma za kisheria kwenye jamii kwa gharama ambazo ni rafiki. Kwa mfano
kuandalia wenye nyumba mikataba ya upangishaji, kuandalia wafanyabiashara
wadogo mikataba ya uajiri, kuwaandalia watu mikataba ya kibiashara na
kadhalika. Kuna taasisi nyingi zinafanya hivi lakini zinawafikia wateja wakubwa
tu, wewe unaweza kuanza na wateja wadogo na ukajenga biashara yako hapo.
Kama unataka
kuingia kwenye biashara hii ya huduma za kitaalamu, jua ile huduma ambayo
unaweza kutoa na anza na wateja ambao hawajafikiwa na watoa huduma waliopo.
Tengeneza jina lako kwa kutoa huduma nzuri na kuza biashara yako kuanzia hapo.
5. Anzisha
na endesha blog.
Blog unaweza
kuitumia kwa biashara zote ambazo tumejadili hapo juu. Unaweza kuitumia kwa
kutoa ushauri wa kitaalamu. Kama wewe ni daktari unaandika kuhusu mambo ya
afya. Kama wewe ni mtaalamu wa rasilimali watu unaweza kuitumia kuandika kuhusu
sifa za kuajiriwa, kudumu kazini, kupandishwa cheo na mengine mengi. Kupitia
yale unayoandika unaweza kutengeneza hadhira ambayo inakufuatilia na baadae
ukageuza blog yako kuwa biashara kwa kutoza huduma unazotoa, kuweka matangazo
au kuuza vitu vyako vingine.