FURSA VIJIJINI,FURSA MIJINI




Tarehe  moja mwezi wa tano 2016, nilienda kijijini Bariadi.Tukiwa kule kijijini mvua kubwa ilinyesha.Kumbe kile kijiji kipo katikati ya mito miwili ambayo yote ilijaa siku hiyo.Hatukuwa na namna isipokuwa kulala kule kule.Tulienda kulala kwa mzee mmoja ambaye alikuwa amejenga nyumba nzuri sana kijijini pale.

Jioni kwenye saa moja hivi alitutembeza kwenye eneo lake. Aisee! nilishangaa sana .Mzee alisema “Nilipoona nipo peke yangu huku porini niliamua kuanzisha center (kijiwe).Nikanunua  mashine ya kusaga unga, nikajenga na maduka ,na nikajenga  godown la kuhifadhia nafaka, na nikajenga na frame za maduka” Mzee alisema.

Mzee huyo ana ukubwa wa eneo lipatalo mamia kadhaa ya ekari, ni kubwa sana.Watu walioona amawekeza hivyo vitu na wengine wakaja wakaanza kununua maeneo yake na kujenga. Sasa hivi ni kamekuwa kamji kakubwa watu ni wengi sana.Serikali imeshapeleka umeme katika kijiji hicho na maeneo yake yote ameshayaandalia ramani za mipango miji huku ametenga eneo kubwa la kuanzisha CHUO.Zaidi ya yote mzee huyu anafuga ng‘ombe kwahiyo maziwa kwake si kitu.Kabla ya umeme alikuwa anatumia umeme wa jua(solar).Kwa sasa mzee huyo amestaafu alikuwa MRATIBU WA ELIMU katika kata yake.

Kwanini nimewashirikisha jambo hili la mzee?. Ni kwa sababu mimi nilijifunza jambo kubwa sana kwake. Kwamba fursa zipo kila mahali mjini na vijijini.Kwa sasa mzee anasubiri tu watu waje kununua viwanja maana tayari ameshavipima na kwa jinsi mahali pale palivyo mzee wa watu atavuna pesa nyingi sana.Nilipojaribu kumdodosa aliwezaje kumiliki eneo kubwa namna ile? Alisema yeye alikuwa ananunua kidogo kidogo na hatimaye akawa na eneo kubwa vile. Kufikiri kwake huyo mzee huenda kuliwa tofauti sana na watu wengi. Chukulia kwa mfano, mimi au wewe tungekuwa huyo mzee,  Je,  tusingekimbilia kujenga mjini na kupaacha kule kijijini?.Kila mtu ajiulize hili swali kama ungekuwa wewe mzee yule ungejenga.

Tunapojifunza kufanikiwa sio tu kutafuta fursa bali pia kubadili mfumo wetu wa kufikiri kuhusu mjini na kijijini.Wengi wa wale wanaoitwa wasomi, akili zao haziwazi fursa zilizopo kijijini bali zimejikita kuwaza fursa za mjini ambazo wakati mwingine ni ghali kuzipata.Ukimwambia leo mtu akaishi Nguruka kule kigoma sijui kama atakubali atajitetea sana, mara nyingi ataanza kusema  si unajua kazi zangu ni za mjini?.

Siku moja nilikuwa nasafiri kutoka Dar kwenda Lindi njiani niliona maeneo makubwa sana lakini hayana watu.Nilipofika nikauliza wenyeji mbona njiani nimeona maeneo makubwa hayana watu?Wakasema yaani huku watu ni wachache sana na kuna maeneo mengine hayana wamiliki.Nilishangaa saana nikasema kweli Tanzania tuna umasikini wa kulogwa .Mifumo tuliyonayo ya kufikiri imetuathiri kwa kiwango kikubwa sana kiasi kwamba kila tunachikiwaza tunafikiria mjini ambako kuna msongamano mkubwa.Mjini sio kubaya ni kuzuri sana ukiweka mambo yako sawa. Lakini tumejisahau kufikiria fursa nyingi zilizopo vijijini.

Kwa mfano mimi nimefika hapa Bariadi mjini sijuani na mtu hata mmoja. Nimekaa nikaona mambo hayaendi lakini kwa kuwa nilikuwa nafahamu siri ya kuangalia fursa mjini na vijijini.Nilianza ziara za vijiji kutafuta maeneo ya kulima bustani.Mahusiano mazuri na wanakijiji yamenifanya nipate ekari 3 za kulima bustani bure.Nimeshalima ekari moja matikiti maji, nyingine nimepanda papai na nyingine najiandaa kupanda vitunguu.Yote hayo nimeyapata bure cha kushangaza kuna wafanyakazi wenzangu ofisini wanajiita wasomi wao habari za vijijini haziwahusu.Sikilizia sasa mziki wake na hivi Maghufuli kabana matumizi, kila siku ni kulalamika.

Ndugu,Umejipangaje kufanikiwa ukiwa mjini na umejipangaje kufanikiwa ukiwa kijijini?Je, siku ukilazimika kuishi kijijini ndo itakuwa mwisho wako wa mafanikio?.Watu wengi nimewaona mara wakihamishwa vituo vyao vya kazi wakapelekwa kijijini ndani ndani kabisa, maisha yao huwa taabu sana kwa sababu hawajajipanga kuona fursa wakiwa kijijini.

Mungu anasema hivi , na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.Kumbukumbu la torati 28:2-3.   Ushauri wangu ni kwamba, hata kama unataka kuanzisha mradi wowote fikiria pande zote uone wapi pana fursa pana na endelevu ikuwa ni mjini au kijijini.Tusilemewe mawazo yetu upande mmoja tu.Ushauri wangu wa pili, jiandae kuishi kila mahali iwe ni mjini au kijiji.Ushauri wangu wa tatu, tunapenda san kuilaumu serikali eti kwa sababu huduma zote inazipeleka Dar.

Wakati tunailaumu serikali tumesahau kwamba hata sisi huduma miradi mingi tunaiweka eneo moja kwa nini tusisambaze miradi yetu?Humu kuna wageni wengi wengine hawanifahamu kwa majina naitwa Mabula Jilala.     


 ~Mabula Jilala