NITAMILIKI BIASHARA YANGU SEHEMU YA SITA



                             NAMNA YA KUPATA MTAJI


Watu wengi wanatamani kuanza biashara lakini wanasingizia kuwa hawana mitaji .Leo Jyb atakueleza mitaji uliyonayo ambayo pengine ulikuwa hufahamu kama unayo na umebaki ukilalamika;


1. Kutumia akili yako (your mind) Kuna watu watapigwa na butwaa lakini ukweli mtaji wa kwanza ulionao ni akili ambayo Mungu alikupa buree kabisa .Huu pengine ndio mtaji mkubwa kuliko mitaji yote duniani bahati mbaya unaweza kuwa ulikuwa hujafahamu na hata mwalimu wako wa chuo kikuu hakukufundisha.

Akili yako ndiyo suluhisho la jambo lolote .Akili yako ndiyo yenye uwezo wa kuzalisha mawazo yenye kuleta mtaji .Ni lazima ili upate mtaji uitumie akili yako vizuri kuwaza kwa kina jinsi ya kupata mtaji vinginevyo utabaki unalalamika.

Kwa mfano kuna mtu anatafuta mtaji wa laki tano wakati huo anamiliki simu ya laki sita, American boot ya laki moja , Nguo za kutosha ,boda boda kila siku n,k .Mtu huyu kakosa mtaji au kakosa akili?.Kwanini asianze kuuza alivyo navyo na kupunguza matumizi apate mtaji?


  2. Kutumia kipaji chako (your talent )
Kipaji chako ni mtaji mkubwa sana ambao Mungu amekupa na kwa bahati mbaya watu huwa hatutaki kujua tuna vipaji gani na hata kama tunajua hatujui kuvitumia na bado tunaendelea kulalamika na kuilalamikia serikali kuwa hatuna mitaji .

Nguvu ya mbegu iko ndani ya mbegu yenyewe hata nguvu,uwezo ,vipawa ,vipaji viko ndani yako lakini umeshindwa kuvitumia na maisha yako yanaonesha hayana mwelekeo kabisa .

Angalia watu ambao shughuli kubwa ni kucheza kwenye maharusi (dancers) na baada ya harusi watu hawa hulipwa kwa sababu ya vipaji vyao na ukweli wanatangeneza hela nyingi sana .Wewe una kipaji gani kikupe fedha??

Angalia wachezaji wa mpira ambao ndio wanaoongoza kwa kulipwa fedha nyingi duniani ni kwa sababu wametumia vipaji vyao walivyopewa na Mungu na vinawalipa sana na chenji inabaki .Wewe ni shahidi kuwa Ronaldo ,Leonal Messi wanalipwa hela nyingi sana .Lakini hapa kwetu Mbwana Sammata ambaye elimu yake siyo kama yako analipwa hela nyingi kwa sababu ya kipaji alichonacho.

Rose Muhando hata sifahamu ana elimu gani lakini jambo ninalofahamu ni kuwa ni mwimbaji maarufu na hapatikani kirahisi bila hela ya kutosha .Nini siri ya Rose Muhando? .Siri ni kuwa aligundua nguvu/uwezo/kipaji chake na akakitumia na sasa kinamlipa .Vipi kuhusu MASANJA?.

Ni lazima ujue una kipaji gani na kukutumia kwa viwango vikubwa na vya tofauti ili kianze kukulipa vinginevyo utabaki kama ulivyo.


     3.Kutumia Ujuzi wako (your skills)
Ujuzi wako ni mtaji mkubwa ulionao .Ni lazima utumie ujuzi ulio nao ili uanze kuzalisha fedha kwa kutumia ujuzi wako vinginevyo utabaki hapo ukilalamika wakati wengine wanatumia ujuzi wao kupiga hatua .

Gerad Saul ni rafiki yangu ambaye alihitimu chuo kikuu IFM  na  shahada ya sayansi ya Bima na udhibiti Majanga (Insurance & Risk Management mwaka 2013 na hakuwa na mtaji lakini akajua kuwa alikuwa na ujuzi wa kushona nguo ujuzi ambao aliupata kwa baba yake .Gerad baada ya kumaliza chuo alifungua sehemu yake ya kushona kwa kuwa mwanzoni alianza kushona kwa watu akapata mtaji na sasa anamiliki kiwanda chake kidogo cha nguo nay eye anashona na shahada yake kichwani

lazima ufahamu kuwa kama una ujuzi, huo ni mtaji wako kabisa hivyo utumia upate fedha kuliko kubaki unalalamika.


4. Kutumia Watu wanaokuzunguka(your network ) Watu wanaokuzunguka ni mtaji kwako ambao Mungu amekupa kabisa lakini bado huna uwezo wa kuwafanya kuwa chanzo cha mtaji wako na umebaki ukilalamika kwa kuwa umekosa maarifa ya kutumia watu wanaokuzunguka.

Watu ndio wenye fedha na kumbe kama watu ndio wenye fedha na wewe umezungukwa na watu hao kwanini unasema umekosa mtaji ?.Shida huna maarifa ya kutosha na wala siyo ukosefu wa mtaji .

Kaa chini angalia watu waliokuzunguka ni watu wa namna gani .Fikiria wazo ambalo linaweza likamfanya huyo ndugu yako atoe fedha kwa ajili yako.Mara nyingi hata ndugu yako anaweza asikupe fedha kama huna bidhaa yoyote ya kumuizia .Ni lazima kuwa na kitu fulani chenye thamani ndipo mtu akupe fedha mbali na hapo huwezi kupata chochote kutoka kwa watu waliokuzunguka .

Kwa mfano kama una mtandao wa watu 1000 wanaokufahamu na ukawa  na wazo zuri lenye mashiko na ukawashawishi watu hawa wakuchangie kiasi cha shillingi elfu kumi tu (10,000/=)  maana yake utakuwa na uwezo wa kukusanya sh milioni kumi ambao ni mtaji mkubwa sana .

Unaweza pia  kutafuta watu ambao wewe unawaamini mkaamua kuchangiana fedha kwa mzunguko .Kwa mfano ukipata watu sita ambao mnaweza kuchangiana shilling laki moja tayari utakuwa na shilling laki sita fedha ambayo unaweza kuitumia kufanya jambo fulani lenye tija .

   5. Kuweka Akiba(Saving )

Siku moja nikasikia mtu ambaye analalamika kuwa hana mtaji wa laki tatu .Mtu huyu kama alikosa mtaji wa laki tatu maana yake kwa siku hakuwa na uwezo wa kuweka shillingi elfu moja kama akiba maana kama ukiweka kila mwisho wa mwaka na alikuwa mfanyakazi wa muda mrefu nilistuka sana siku sh 1000 kwa siku miatatu sitinI na sita kwa mwaka inakuwa laki tatu na sitini na kama unaweka 2000 unapata laki saba na kama unaweka elfu tatu kila siku kwa mwaka utapata milioni moja.

Nilivyopiga mahesabu haya niligundua kuwa tunapoteza hela nyingi sana na tumekuwa na kasumba ya kudharau hela ndogo na tumebaki tukilalamika .2017 amua kuweka nidhamu ya fedha ili uanzishe biashara yako kabla mwaka haujaisha .Ukweli tumekuwa tukipata fedha lakini tumeshindwa kuzitumia vyema maana hatuna mipango hata kama majukumu tunayo mengi .

 6. Kubadilisha unavyomiliki kwenda kwenye fedha(converting things into money )

Moja ya namna ya kupata mtaji ni pamoja na kuuza ulivyo navyo  ili upate fedha za kukusaidia kuanzisha biashara .Kwa mfano kama una simu ya laki tatu na nusu na unatafuta mtaji wa sh laki mbili na nusu kwanini usiuze simu yako hiyo ufanye biashara ili baadae ukianza kupata faida uweze kununua simu nyingine.

Kuna vitu vingi tunavyo vya anasa ambavyo tunatumia pesa nyingi kuvinunua wakati fedha hizo ndizo zingetusaidia kupata mtaji wa kuanzia kwenye biashara zetu.

Joas