Kwani wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini?
Katika jamii ya waswahili huu ni msemo ambao umekuwa ukitumika sana na ni miongoni mwa misemo ambayo imejipatia umaarufu mkubwa sana. Ni kweli kuwa wapo watu wafanyao mambo makubwa na yakatokea lakini wengine hushindwa kufanya mambo hayo. Wafanikiwao nao ni watu kama walivyo watu wengine ila utofauti mkubwa hujengwa katika namna ya kufikiria na pia katika namna ya kufanya mambo. Watu wote walio juu ukifuatilia historia zao utakuta walikuwa ni watu wa kawaida sana, ila ndani yao waliweka nia na kuamua kupambana kufikia hatua kubwa na za juu, na watu wa namna hii hata walipopata mafanikio madogo hawakubweteka na kujisahau bali walizidi kusonga mbele kupata mafanikio makubwa zaidi. Kama wao wamejaribu wakaweza kwa kutia nia na wewe ukitia nia kwa lolote ufanyalo ni lazima utaweza tu.
Mfumo wa kuzaa kwa viumbe
Nikiwa na rafiki yangu tunazungumza na kutiana moyo kwa habari ya safari tuliyonayo akazungumza neno jema sana kuhusu maono kwa kufananisha na wanyama, kuwa wanyama wadogo hubeba mimba na kujifungua kwa muda mfupi; wengine hubeba kwa miezi mitatu (3), wengine ni sita (6) na wengine ni tisa (9), tofauti huwa kwa wanyama wakubwa kama tembo wao hubeba mimba yao kwa muda mrefu sana ukilinganisha na wanyama wengine, hii ni kwa sababu ya ile asili yao ya ukubwa ambayo Mungu amewawekea.
Kwa kuutazama mfano huu ndivyo ilivyo kwa sisi wanadamu ya kuwa maono makubwa huweza chukua muda mrefu sana kabla ya kutoka na mtu mwenye maono makubwa huchukua muda mrefu pia kufikia utimilifu wa maono yale. Usiumie kwa nini wengine wanatoka upesi na wewe unapambana ila bado; fahamu aina ya maono uliyobeba pengine ni mazito kama mimba ya tembo na kama ndivyo yaweza kaa muda mrefu hata utimilifu wake ila yatatokea tu kwa kuwa maono ni kama mimba.
Mbali na wanyama pia kwa mimea kuna neno jema la kujifunza kwa kuwa kuna miti ambayo hupandwa na kukua kwa muda mfupi na huvunwa ndani ya muda mfupi huo, ila kuna mimea ambayo hukaa sana na huchukua miaka mingi sana hata kufikia utimilifu wake, kwa kuchukulia mifano kama mnazi, hata mbuyu hukaa kwa kitambo kirefu sana hata kuja kutoa matunda yake.
Hii inaonyesha kuna utofauti mkubwa sana wa utimilifu wa maono ya mtu mmoja mpaka mwingine, kuna wengine ambao hushuhudia utimilifu wa maono yao kwa haraka sana ukilinganisha na wengine. Muda wa kuchelewa kwa maono ya mtu Ibilisi huutumia sana kuwa shawishi watu kuona kuwa Mungu hayupo pamoja nao, na huweza kusema, mbona hujabarikiwa kama fulani na fulani na wewe unamtumikia Mungu kama wao, au ulimaliza nao chuoni au shuleni au ni marafiki wa karibu ukishiriki nao mengi sana ila wao wamekupita kufanikiwa kwa kuwa Mungu hajali mambo yako na huwapenda wenzako kuliko wewe; wewe usikatishwe tamaa na sauti ya kinyonge namna hiyo songa mbele maana utimilifu wako unakuja na ufanikiwaji wa mtu mmoja na mwingine huwa tofauti na kwa nyakati tofauti tofauti.
Mtu mwenye maono hawezi kutulia hata atimize maono aliyonayo na hata akishindwa mara moja huinuka na kujitia nguvu na kutokata tamaa na ni maono ambayo humsaidia mtu kuishi kwa kuukomboa wakati, kuweka vipaumbele vya maisha ambavyo vitampelekea kufikia utimilifu wa maono hayo, kuchagua watu sahihi wa kuambatana nao ambao watamsaidia kufikia hatima ya maisha yake.
Kutokuwa na vipaumbele katika maisha.
Kukosa maono kunapelekea mtu kushindwa kujizuia na huku kushindwa kujizuia ndiko kunamaanisha kutokuwa na vipaumbele. Mtu yeyote mwenye maono ni lazima atakuwa na vipaumbele vya msingi katika maisha yake na vipaumbele hivyo humsababisha kufikia utimilifu wa maono aliyonayo.
Vipaumbele ni vitu ambavyo hupewa umuhimu wa hali ya juu na hupewa umakini mkubwa zaidi ya vitu vingine vyote. Na vitu hivi huweza kuchukua muda mwingi wa mtu kuliko vitu vingine vyote na mtu huwa makini sana kutoruhusu vitu vingine ambavyo vitaharibu utaratibu uliopo. Vipaumbele husababisha utimilifu wa maono aliyonayo mtu na humfanya mtu kuzingatia kuwa sehemu sahihi, wakati sahihi na watu sahihi.
Kwa mfano mwanafunzi awapo shuleni ni lazima awe na vipaumbele vya msingi kama kumtumikia Mungu kama balozi wa Yesu katika eneo asomalo na kusoma kwa bidii zote, kwa kuwa ni jukumu la msingi pia lililompa kuwepo mahali hapo. Na si kwa wanafunzi tu bali hata aliyepo kazini ni lazima awe na vipaumbele vya msingi vitakavyomsababishia kufanikiwa katika kufikia hatima yake iliyo njema.
Asiye na vipaumbele hufanya mambo yake pasipo mpangilio na huwa ni mtu asiye na misimamo juu ya yale ayafanyayo na hukosa kujitoa kikamilifu katika mambo ayafanyayo.
Katika vipaumbele ni vyema kuzingatia kuwa kila jambo katika ulimwengu huu lina majira yake, na nyakati zake na utambuzi huu utamfanya mtu kufanya kitu sahihi katika wakati sahihi na kuepuka kufanya jambo ambalo lipo nje ya wakati.
Mambo ya msingi katika kufanikisha vipaumbele vyako.
- Chagua marafiki sahihi.
- Kuwa mahali sahihi, sehemu sahihi na ukifanya jambo sahihi.
- Kila jambo ulifanyalo zingatia wakati kwa kuwa kila jambo lina wakati wake na majira yake/ukomboe wakati.
- Ishi kwa malengo, timiza malengo yako.
- Usiishi maisha ya kuigiza, ishi maisha yako.
- Tumia vyema fedha uzipatazo hata kuweka akiba ya kukusaidia baadae.
- Kuwa hodari na moyo wa ushujaa/ usiogope kwa kuwa yapo mengi yaogopeshayo ila sababu ya kutoogopa ni kuu zaidi ya hayo yote.
- Mwamini Mungu.
- Jiamini wewe mwenyewe kuwa unaweza.
Mungu Anaona Ambayo Wengine hawaoni juu yako.
Ikiwa Mungu aliona taifa kubwa ndani ya Yakobo mchunga mifugo wa Labani, akaona Waziri Mkuu ndani ya Yusufu mfanya kazi wa ndani na mfungwa kule Misri, akaona mkombozi wa Israeli kwa Musa mchunga mifugo kule Midiani kwa Kuhani Yethro, Akamwona Mwamuzi wa Israeli Gideoni yeye Ambaye alikuwa dhaifu na kutoka katika familia ya hali ya chini sana, Akamwona Yefta aliyekataliwa na ndugu zake na kumfanya kuwa mwamuzi wa wana wa Israeli, Akaona Mfalme wa Israeli ndani ya Daudi Mchunga mifugo na hakutazamiwa hata na baba yake, Akaona Mwokozi wa ulimwengu na Mfalme wa mataifa katika Zizi la Ng’ombe (Yesu). Leo hauzuiwi na hali uliyonayo wewe kukufanya mtu mkubwa, usiache kumtumaini ni lazima atafanya alichokusudia kwako.