"Maisha yako ni bustani na wewe ndiwe mtunza bustani hiyo. Unaweza ukaamua kuipalilia na kuimwagilia maji au ukaamua kuiacha iote magugu na ikachakaa".
Katika kila maamuzi unayoyafanya kila iitwapo leo lazima kuna matokeo yake siku za usoni. Maisha unayoishi leo kwa sehemu kubwa ni matokeo ya maamuzi uliyoyafanya hapo nyuma.
Dunia inaundwa na makundi nne(4) ya watu na haya makundi ndio huleta maana halisi ya maisha.
1.WACHEZAJI.
Kama maisha yangekuwa mchezo wa mpira basi hawa ni watu au wachezaji walioko ndani ya uwanja. Hawa ni wale ambao hukabiliana na hatari, huchukua hatua, hutumia nguvu na juhudi kadri Mungu anavyowawezesha kufikia ndoto na malengo yao.
Hili ni kundi ambalo hutumia muda na nguvu kufanya yale yaliyoko moyoni. Ni watu ambao wanaishi katika ndoto na shauku ya kufikia matamanio ya mioyo yao. Hawa ni watu mashuhuri na maarufu duniani. Hili ni kundi la viongozi wakubwa, wafanyabiashara wakubwa, wanasoka wakubwa, wanamuziki wakubwa, waandishi wakubwa, wasomi wakubwa. Hili kundi la washindi na mashujaa.
2.WATAMAZAJI
Hili ni kundi lingine ambalo watu wake hukaa pembeni na kutazama wachezaji wakicheza mchezo wa maisha. Hukaa pembeni na kuishia kuangalia wengine wakipata umaarufu, pesa, mafanikio. Kazi yao ni kuzungumza kuhusu watu wengine. Wanaona kile ambacho wengine wapo wanafanya lakini wao hawafanyi, hawa wana ndoto ya kuwa wachezaji lakini hawawezi kujaribu kufanya kitu kipya, hususani vile vitu vigumu.
Wanatamani sana kuingia kwenye mchezo wa maisha lakini hawaingii. Wanaishia kujutia. Utasikia, "ningefanya vile na mimi ningekuwa na maisha mazuri kama fulani". Hawa watu wamechukua viti na wamekaa wanawatazama wenzao wakicheza mchezo wa maisha ambao hata wao wana wajibu wa kuucheza. Hata wakijaribu kucheza wakikutana na changamoto kidogo hukata tamaa na kuendelea kuwa watu wa kawaida.
3.WASHANGILIAJI.
Hawa wako nje kabisa ya uwanja wa mchezo wa maisha. Wao husikia umbea kutoka kwa watazamaji, wao huwa sio sehemu ya mchezo. Hili ni kundi la watu ambao huishi katika ulimwengu usio na hisia, shauku, malengo na ndoto. Huishi katika dunia ya ingekuwa, ningekuwa, wangekuwa, angekuwa. Wanasikia sauti za wachezaji na watazamaji lakini hawaoni.
Wanajua kuwa kuna kitu kinachoendelea katika uwanja wa maisha lakini hawafikirii hata kwenda kuangalia ni kitu gani kinachoendelea. Hawajui kama hawajui kwa hiyo hawako tayari kujifunza.
4.WASHANGAAJI.
Hili ni kundi la wale ambao wamepotea njia katika maisha. Wako stendi lakini hawajui wapande gari gani na waelekee wapi. Hawa ni wale ambao maisha yamewaacha. Hawaishi ila wanapumua. Wapo ulimwengu mwingine kabisa.
Kundi hili linaendeshwa na "addiction"(waliothirika) labda na pombe kali, madawa ya kulevya kama unga, bangi, cocaine. Hili kundi la wale walio poteza mwelekeo, waliokata tamaa, kundi la wasio tumaini kesho iliyobora. Hili ni kundi la watu wanaoshangaa shangaa jinsi ulimwengu unavyoenda bila kujua hata sheria moja ya mchezo wa maisha. Hawa watu wana mikono lakini hawashiki, wana ubongo lakini hawafikirii, wana macho lakini hawaoni, wana maskio lakini hawaskii, wana miguu lakini hawatembei,...... Kwao maisha ni Giza na wanaufahamu mdogo sana kuhusu maisha. Imani yao ni finyu sana na hawaamini katika mabadiliko.
wewe unahisi upo katika kundi gani kati ya hayo manne?
"Badilika Au Kufa".