MAMBO 10 USIYOYAJUA KUHUSU MATAJIRI ~Kashindi Edson

                        




“Ukimuona kuku kwa mganga ujue kilichomponza rangi yake”. Kataa au kubali kuwa hapo ulipo leo hii kunapelekewa na sababu fulani fulani ambazo unazifahamu au huzifahamu. Vivyo hivyo kuwa katika kundi la maskini au katika kundi la matajiri kunasababishwa na mambo kadhaa.

“Utajiri” ni sawa na  “Sumaku”, Sumaku huvivuta vitu vyenye asili ya chuma, na kuvisukuma au kuvikataa vitu visivyo na asili ya chuma kama vile plastiki, mbao, karatasi. Ili upate utajiri  (Mafanikio ya kipesa) unahitaji kuwa na tabia zinazovutwa au kuendana na utajiri. “Kuna watu fulani, kulingana na tabia zao hawawezi kufanikiwa”-Eric Shigongo.

Watu walio na mafanikio makubwa ya kipesa huwa maisha yao yana mambo kadhaa ambayo maskini hawana. Katika makala haya tumekuandalia vitu 10 usivyovijua kuhusu maisha ya matajiri wakubwa duniani.

1.Matajiri Wote Wamejiajiri. “Kutegemea mshahara pekee kama chanzo cha utajiri au mafanikio ya kipesa ni sawa na kipofu anayevuka barabara”. Hakuna mtu aliyepata mafanikio makubwa ya kipesa kwa kutegemea mshahara. Watu wote wenye mafanikio makubwa ya kipesa tunaowaita matajiri leo hii wanafanya biashara na shughuli zao binafsi. Historia inaonesha kuwa, matajiri wengi waliachana na ajira kabla ya kuwa hapo walipo leo.

2.Matajiri Wote Wanajifunza Kila Siku. Wao huwa ni wanafunzi wa mafanikio kila muda. Hutafuta maarifa mapya kila siku, hutafuta taarifa mpya, masikini yeye anahisi anajua kila kitu swala ambalo sio kweli. Matajiri wengi wamekuwa ni wasomaji wa vitabu vya maendeleo binafsi, “personal development books”, vitabu kama vile Bible, Quran, Think & Grow Rich, Law of Success, Rich Dad Poor Dad, nk. Wengi ambao hatujafanikiwa huwa hatujishughulishi hata kidogo katika kujifunza, nadhani hicho ndo kinachopelekea uwepo wa maskini na tajiri.

3.Matajiri Wote Wana Mitazamo Chanya. Chuki, Vinyongo, vipo akilini mwa watu masikini. Tajiri hana muda na hizo habari. Ndio maana tajiri yupo karibu na tajiri, maskini yuko pekee yake. Matajiri wote wamekuwa wakiwashauri watu wote kuwa chanya na kuepuka mitazamo hasi kwani inapingana na mafanikio ya aina yoyote hata ya kiimani.

4.Matajiri Wote Wana Vyanzo Vya Pesa Zaidi ya Viwili. Hakuna tajiri yoyote aliyefanikwa kwa kuwa na chanzo kimoja cha pesa. Wengi wao huwa ni wawekezaji katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi, matajiri wengi wanamiliki makampuni kuanzia mawili. Ni masikini pekee anayetegemea chanzo kimoja tu cha pesa. Mtu ana duka moja, ukimwambia apambane aongeze duka la pili anahisi unamdanganya.

5.Matajiri Wote Hawalalamiki. Ni masikini peke yake anayeilalamikia serikali, mwalimu, mchungaji, familia, ndugu, na marafiki. “Mtu anayehitajika kufanya kile unachohitaji kifanyike katika maisha yako ni wewe”-Dr Ben Carson. Watu wenye mafanikio makubwa ya kipesa, huamini kuwa, “wana nafasi kubwa ya kubadilisha maisha yao wao wenyewe kuliko mtu yeyote mwingine”. Mafanikio uliyonayo ni matokeo leo, yanatokana na wewe mwenyewe sio mtu mwingine.

6.Matajiri Hawajutii Kuwa Pale Walipo. Tajiri hajutii kuwa tajiri, siku zote hujivunia kuwa tajiri. Hata ukisema lolote baya juu yako, hatajuta hata siku moja. Kuwa tajiri au maskini ni maamuzi ndo maana wao huwa hawajutii.

7.Kwao Kila Kitu Kinawezekana. Neno haiwezekani kwao halina nguvu hata kidogo. Maskini ndo anayeishi na neno haiwezekani. Neno Haiwezekani lipo kwenye Kamusi ya Wapumbavu. Matajiri huwa wanaishi kwa Imani kubwa sana kumshinda hata Mchungaji au Shehe. Wanaamini kuwa kila kitu kinawezekana hasa kwa kujiangalia wao wenyewe walipotoka na walipo muda huu. Tajiri yeyoye sio mwoga, anachoogopa ni woga wenyewe.

8.Matajiri Wanalala Masaa Machache Sana. Watu huwa wanajiuliliza mbona ni kazi sana kukutana na matajiri?, Jibu rahisi tu, huwa wako “busy”. Kama maskini anashinda kitandani amelala eti kakosa kazi ya kufanya, tajiri yeyeye huwa hana hata muda wa kulala. Matajiri wote huwa wanafanya “kazi sana” kwa masaa mengi. “Ukilala sana unavuna ulichokiota”. Matajiri wote wanabidii na juhudi kubwa katika kufanya kazi. “Uvivu hulipa leo, juhudi hulipa baadae” kwa hiyo inabidi kuchagua kulipwa leo au baadae ingawa matajiri huchagua kulipwa baadae.

9.Matajiri Wanaiona Baadae Yao Kabla Ya Kuifikia. Matajiri huishi na ndoto, maono na matamanio.  Huwa na malengo, hatua na mikakati inayowapeleka kule wanakotaka kwenda. Hufanya kazi usiku na mchana kufuata ndoto na maono yao. Huamini sana katika ndoto na maono. Huamini katika malengo. 

10.Tajiri Si Rafiki Wa Mtu Yeyote. “Rafiki wa wote si rafiki wa mtu”-Plato. Matajiri hawapendi urafiki na kila mtu, huunda urafiki wenye manufaa ya kibiashara tu. Hawana muda wa kupiga domo na stori za kijinga. Tajiri hana marafiki wengi, ila marafiki wachache wenye manufaa makubwa katika maisha yake. Wakati mwingine matajiri huwa wanapenda kuwa pekee yao huku wakitafuta mawazo mapya ya kibiashara.

 Pia ubunifu, umakini, matumizi mazuri ya pesa, na nidhamu ya maisha huzingatiwa sana na matajiri kwa sehemu kubwa.
“Utajiri ni matokeo ya tabia na vitendo vya mwanadamu katika maisha yake ya kila siku”

                                    

Thanks A lot , Wish You Successful and Strong Future.