MAMBO YATAKAYOFANYA BIASHARA, KAMPUNI, NA TAASISI UNAYOIANZISHA ISIDHOOFIKE NA KUFA

Pata kitabu hiki kwa bei ya sh elfu tano tu (5,000/= 0713804078


1


USIANZE MPAKA UWE NA TAARIFA ZA KUTOSHA

Wengi huanzisha biashara kwa kuwaiga watu wao wa karibu na huanza bila kufanya utafiti wa kutosha kuhusiana na hizo biashara. Yawezekana hufanya hivyo kwa kuwaiga tu wale wanaofanya au wamewaona watu fulani wakiwa wanafanya nao wakaamua kujiunga nao.

Kuna wakati Bwana Yesu akiwa anafundisha akawaeleza wanafunzi wake kuwa mtu yeyote akitaka kujenga mnara ni muhimu akae chini na kupiga hesabu (cost calculation) kama anavyo vya kuumalizia? asije kuishia katikati na watu wakaanza kumcheka kuwa alianza kwa kasi sasa kasi yake ipo wapi, rejea kitabu cha Luka 14:28-30.

Maana yake kabla hujafanya kitu chochote ni lazima uketi chini (utulie) na kupiga hesabu (kuwa na mipango na mikakati ya kueleweka) na ndipo mtu aweze kuanza anachoanza. Kama mtu hatoweza kufanya hivyo ni dhahiri ataanza ila hatoweza kufika mahali popote.Wapo vijana wengi sana ambao wanajihusisha kufanya vitu ambavyo hawana taarifa navyo kabisa.Usianze kufanya mpaka umepata taarifa za kutosha.

Wakati namaliza chuo mwaka wa tatu kila mmoja alikuwa katika mchakato wa kutafuta sehemu ambayo atafanya kazi ya kumpatia kipato kizuri, wengi walijihusisha na kufungua taasisi (CSOs) kutokana na taarifa ambazo zilikuwa zikienea kuwa mkiwa na CSOs yenu serikali itakuwa inatoa ruzuku ya kuanzia na wengi wakaamua kuanzisha hizo taasisi lakini baada ya muda mfupi tu taasisi zile zilikufa na kubakia kwenye makaratasi. Watu walikuwa na shauku ya kuanzisha ila maarifa ndio ilikuwa tatizo.
Tafuta taarifa kwa kadri uwezavyo, fuatilia watu mbali mbali waliowahi kufanya na uwaulize ili upate taarifa zitakazokusaidia nawe kufanya kwako.

Nyakati za hivi karibuni kumetokea wimbi kubwa la ufugaji wa sungura na ilipotangazwa kuwa katika kufuga sungura kuna faida kubwa wapo watu wengi sana wakakimbilia kufuga sungura ili kuuza nje ya nchi ila matokeo yake yalionekana kuwa wengi walifanya ila wakapata faida kidogo na wengine hawakupata kabisa kwa sababu tu walifanya ila hawakuwa na taarifa za kutosha.

Mwaka 2016 tulishuhudia wimbi kubwa la wakulima wa nyanya wakipata hasara kubwa sana kwa kuuza tenga moja shilingi 700/= na wengine kuona ni bora wakawapa ng’ombe na nguruwe wakala kuliko hasara waliyoipata. Suala kama hili wengi waliishia kuilaumu serikali kuwa haijawatengenezea mazingira ya soko na viwanda rafiki vya zao hilo kama vile vya usindikaji. Nina uhakika kama wangeuza shilingi 50,000/= kwa tenga, hizi lawama tusingezisikia. Ukitafakari utagundua wengi hufanya kilimo kwa ufinyu wa taarifa na sio watafiti kabisa, na wengi huwa wanapigia mahesabu faida wanayopaswa kuipata na huwa hawana tahadhari ya upande hasi. Wengi walilima nyanya kwa sababu walisikia rafiki au ndugu zao wakiwaambia kilimo cha nyanya kinalipa sana.

Katika eneo hili ni muhimu sana kuzingatia upataji wa taarifa za kutosha kabla ya kuanza. Ukiona watu wengi wanajihusisha na kulima matikiti ni lazima ufahamu kuwa matikiti yanakwenda kushuka bei sokoni kwa kuwa yatakuwa yanapatikana kwa wingi zaidi, na ndicho kinawakumba watu wanaambiwa wakilima zao fulani lina faida sana na unakuta karibia wote wanaingia huko na kusahau mazao mengine. Ukweli ni kuwa kila zao linalipa ila inategemea unafanya kwa namna gani.

Nimeona watu wengi sana wakiigana bila hata ya kuwa na taarifa, yaani kila mtu anataka kufanya kitu kile kile anachofanya mwingine mwisho wa siku wanaofanya biashara za namna hiyo wanakuwa wengi na kupoteza kabisa soko. Kabla hujaanza piga hesabu na usifanye kwa sababu fulani anafanya, wewe fanya kwa kuwa unaona unamudu kufanya hiyo biashara.Kuna nyakati watu wengi walifanya kwa kuigana kuanzisha biashara za m-pesa, tigo pesa, airtel money na baada ya muda mfupi wengi wakaanza kuacha na kurudi nyuma na kuona ni biashara ngumu kwa sababu hawakupiga hesabu. Wengine walikuwa wakikosa wateja maana mabanda yakawa mengi kuliko huitaji.

Duniani hakuna kitu kigumu wala kitu kirahisi, ugumu au rahisi wa kitu unategemea na mtu mwenyewe. Kile unachokiona kigumu sana kuna mwingine ndicho anaona ni rahisi zaidi na kile unachokiona kirahisi kuna mtu anakiona ni kigumu sana. Ni wewe ndiye unaweza kufanya biashara yako, kampuni yako, na taasisi yako vionekane vigumu kutekelezeka au vikawa vyepesi.Taarifa za juu juu zinasababisha wengine kuwa na matarajio ya juu sana ‘too much expectations’ na mambo yanapowageukiwa na kuwa ndivyo sivyo hujikuta katika hali ya kukata tamaa na kuamua kuachana na vile walivyovianzisha.




2

USISHINDANE NA MTU, SHINDANA NA MAONO YAKO

Watu wengi hupenda mashindano, na mambo mengi sana hufanyika kwa mashindano. Mashindano hayo hupelekea wivu na wakati mwingine chuki na maneno mabaya haswa pale mshindanaji anapohisi kushindwa. Watu waliofanikiwa na wanaofanikiwa duniani kote ni watu wanaohangaika kutekeleza maono yao usiku na mchana na si watu wa kuhangaika kushindana na wengine, na ni nadra sana kuwakuta wakizungumzia watu wengine kwa namna ya kuwakosoa ili wao waonekane ni bora zaidi ya hao watu. Ukiwakuta wanafuatilia watu wengine hufuatilia kwa kutaka kujifunza na kuhamasika na si kutaka kuiga.

Ni jambo la kawaida sana ukamkuta mtu ameamua kununua gari kwa sababu rafiki yake amenunua na anashindwa kuangalia vipaumbele. Simaanishi kununua gari ni tatizo, tatizo ni kukosa vipaumbele vya msingi. Au ukamkuta mtu anakosoa kazi ya mwingine ili tu yeye aonekane ni bora zaidi ya huyo mtu.

Usishindane na mtu maishani mwako, hujui huyo unayeshindana nae ametokea wapi, na anaelekea wapi, kamwe usiige mwendo wa mwenzio lakini hamasika kwenye mwendo wa mwenzio. Kila mtu anamwendo wake na ana sehemu anayopaswa kufikia, mara zote hangaikia kufika kwenye ule mwendo unaopaswa kufikia.

Wakati nasoma chuo kikuu cha Dar es salaam nilikuwa na rafiki yangu ambaye pia alikuwa ndiye katibu wangu nami nikiwa mwenyekiti katika fellowship ya kuabudu pale chuoni. Kila siku tulipokuwa tukimaliza ibada alisalimia watu na kisha kuondoka, alikuwa anatembea mwendo wa kasi sana na wakati mwingine ulikuwa ukitaka kuongozana nae ungemuacha tu akutangulie kwa sababu kasi yake ilikuwa kubwa akiwahi majukumuni mwake, nafikiri alifahamu vyema sana kuwa kuna majukumu yanamsubiri sehemu fulani na ndiyo maana alikuwa akifanya upesi kuyaelekea. Ule mwendo ulikuwa mgumu sana kwa wengi kwa kuwa kama ungetaka kumuiga mngeweza kufika lakini ukiwa umechoka ila yeye asingechoka kama wewe kwa kuwa anaumudu na ndio mwendo wake, na pia mkifika unaweza ukajikuta hata viatu vyako vipo katika hali mbaya kwa sababu ulitembea katika mwendo ambao siyo wako. Ni vyema ukajifunza kutembea katika mwendo wako katika ustadi na unadhifu huku ukijua ni wapi unaelekea.

Kuna mtu aliyekuwa ameamka kufanya mazoezi ya asubuhi kwa kukimbia barabarani, wakati anakimbia aliona mtu mbele yake akiwa amemuacha mbali sana, akaamua kuanza kumfukuzia, alimfukuzia mpaka akamkuta, alipomkuta akazidi kukazana hata alipompita kabisa ndipo alipojisikia vyema na baada ya kukimbia tena umbali mdogo akaona yule mtu anakata kona anaingia nyumbani kwake kwa maana ameshafika mwendo wake, naye akawa amebakia peke yake barabarani.

Fahamu ya kuwa kila mtu ana mwendo wake na ana kituo chake anachopaswa kwenda, usiige mwendo wa mwenzio na wala usishindane nae, ila waweza kuhamasika kwa namna anavyotenda.Usimkosoe mtu ili wewe uonekane ni bora zaidi yake. Kuna ambao huamini kuwa wakiwapaka wengine matope basi hujisafisha na kuwa safi, ila ukweli ni kuwa mtu bora ni bora tu hata ukimpaka matope atang’aa tu.
Na huwezi kuwa bora kwa kukosoa walio bora au kuwa bora kwa kushindana na walio bora ila unaweza kuwa bora kwa kuwapenda, kuwakubali, kujifunza kwao na kuwa karibu nao.

Usishindane na mtu maishani mwako, mara zote angalia kusonga mbele na tafuta mambo yatakayokufanya kuwa bora na usonge mbele daima ili utimize malengo uliyojiwekea.Maono yako katika kitu ulichokianzisha ni ya muhimu sana zaidi ya kushindana na watu. Wakati wote palilia na kuyaatamia maono yako.Hii Ndiyo Kanuni:

·        Macho yako yatazame picha ya ndani siku zote ya kule unakoelekea
Ukiwa na picha ya taasisi, biashara, kampuni yako inavyopaswa kuwa basi ni muhimu macho yako yaitazame ile picha zaidi ya picha iliyopo sasa katika mazingira yaliyokuzunguka. Kama hauna picha ya kule unapoelekea basi inakuwa rahisi sana kuchanganywa na yale unayoyaona sasa katika mazingira yako sasa.

Kama unafanya uzalishaji wa chillsource uwe na picha ndani yako kuwa siku moja lazima nije kuwa na kiwanda kikubwa Tanzania, Afrika na Ulimwenguni ambacho kitakuwa kinajihusisha na uzalishaji wa biashara hiyo. Au kama unashona nguo kuwa na picha ya kuja kumiliki kiwanda kikubwa cha ushonaji kuanzia nchini mpaka nje ya nchi na ndicho kitu muhimu zaidi kukifanyia kazi usiku na mchana.  

Ona mbali zaidi ya mambo yako ya sasa yanavyoonekana, usiwe na uonaji unaodhibitiwa na mazingira yaliyopo. Hata kama unatumia brenda kuzalisha juisi unayozalisha sasa, tazama kama mtu ambaye anajua kuwa hajafika. Endelea kuona kuwa siku moja wewe utakuwa ni mtu anayezalisha juisi nzuri zaidi ya wazalishaji wote tulionao leo.

Ijapokuwa mwanzo wako ni mdogo inawezekana mwisho wako utakuwa mkubwa.
Fanyia kazi ile picha unayoiona na usihangaike na mashindano na watu unaowaona. Kataa kuongozwa na maisha ya wengine, maisha yako yaamriwe na kuongozwa na aina ya maono uliyonayo kwa sababu kila mtu anamwendo wake.

Usiige miendo ya watu kuna wengine hawaendi mbali kama unapoelekea wewe na ndio maana wanatembea taratibu, ukiiga unadhani eti mnachelewa wote kumbe unayechelewa ni wewe. Kuna wengine muda wao wa kufika ni saa saba japo wameanza safari mapema zaidi usijidhanie kuwa uko nao wewe wa saa sita piga mwendo zaidi yao.

Wengi sana hupenda kufanya kama fulani anavyofanya kwa kudhania huo ndio mfumo wa marafiki. Kataa hali ya namna hiyo, kila mmoja ana maono yake. Toa kipaumbele kwenye mambo ya msingi tu yatakayokufanya ufikie yale malengo uliyonayo.

·        Masikio yako yasikilize sauti ya kule unapoelekea zaidi.

Kuna tofauti kati ya kusikia na kusikiliza, unaweza ukasikia lakini ukashindwa kusikiliza.
Yape masikio yako kusikiliza sauti ya maono yako japo yatasikia sauti nyingi ila yape kusikiliza (umakini) ile sauti ambayo imebeba kesho yako.Ukiyapa kusikiliza yanayotokana na mazingira uliyopo sasa yanaweza kupeleka taarifa ya kukatisha tamaa katika moyo.

Watu wanaweza kukusemea wewe kwa vile unavyoonekana leo ila sauti ya ndani ndiyo inaweza kukutambulisha wapi unaelekea, usiishie kwenye wigo wa watu wanavyoona, ona kwa jicho la ndani lionalo maono yako.Wakati fulani nilitafuta mshauri (mentor)ili anisaidie ushauri wa ndani kuhusiana na shughuli ninazozifanya katika kampuni yangu ya Gracious Printing Press.   Nilipokutana naye nilimuelezea kule napopaswa kufikia na aina ya hatua ambazo nimekuwa nikichukua ili kufikia, aliposikia akanitazama kwa muonekano wa nje na kuona sitoweza kufika haswa kama nitafanyia biashara hapa Dar es salaam, akaona anishauri nifanye biashara nyingine na kama nafikiria aina ya biashara hii ni lazima nifikirie kutoka nje ya Dar es salaam ambapo hakuna ushindani mkubwa.

Alichoona labda sitoweza ushindani uliopo Dar es salaam, lakini mimi nilikuwa naona kampuni kubwa sana na naamini kwenye ushindani wa kibiashara ndipo kwenye ubora na mafanikio na ndiyo sehemu ambapo akili hufanya kazi zaidi ya kawaida. Nilimsikiliza ila nilipoona ushauri wake unakinzana na safari yangu nikaona niendelee mbele tu kiutendaji.

Pata Mengi kupitia Kitabu chake kinachoeleza kwa kina Mpigie Kelvin Kitaso kwa namba hizi 0713804078 bei ni shillingi elfu tano tu (5,000/=)