Kifungashio cha siku ya Valentine sehemu ya kwanza...~ Ushindi Elioth






Leo ni tarehe mosi Februari. Na leo ndio siku ile tunaanza mfululizo wa siku 14 ambazo nitakushirikisha mambo ya msingi katika kuimarisha mahusiano hususani katika ndoa. Mtazamo wa fundisho hili ni ule unaotokana na fundisho la Biblia.
Kwa sababu ya changamoto zilizopo katika mahusiano,ndoa nyingi zimeingia katika matatizo, kuvunjika na zingine zinaendeleana kuvumilia yaani mithili ya kuota moto mkali kwenye jua. Lengo la kuandaa mfululizo huu ni kuona huba na upendo katika ndoa vinarejea,ninaamini kwa msaada wa Mungu na fundisho sahihi juu ya ndoa inawezekana.

Ndoa zilizo na furaha,amani na upendo zinawezekana.Leo kwa kuanzia ningependa nikutazamishe mambo kadhaa ambayo ni chanzo cha migogoro mingi katika mahusiano. Nitayaainisha na haya nitaendelea nayo kwa siku 14 zilizobaki. Mambo hayo ni mtazamo (attitude),Wajibu, matarajio, mawasiliano, ufahamu,na commitments. Haya mambo ndiyo hasa kiini cha migogoro na tofauti zinazoendelea kutesa na kuharibu mahusiano.
 
Mtu mwenye nafasi ya kuwa na ndoa bora yenye staha ni yule anayekubali kujipatia ufahamu kwa kujifunza, kujifunza kwa upya na kujifunzua (Unlearn) kuhusiana na mahusiano. Kama tukitia juhudi katika kutafuta maarifa ili kuwa na mahusiano yenye tija inawezekana (Nancy Van Pert).

Jambo la kwanza: Kwa nini unaoa / Olewa?
Umewahi kujiuliza swali hili? Kama ndiyo ulipata majibu gani? Na kama sio chukua dakika 5 utafakari ni sababu gani ya msingi inakufanya uoe au kuolewa,au ilifanya uoe /uolewe.

Majibu kwa swali hili yanaonesha msukumo nyuma ya tendo,na msukumo huo hutoshelezwa na lile jibu kwa kusudio nyuma yake. Inapotokea kusudio halipati majibu tayari mgogoro unaanza kujitokeza. 

Unapokuwa una njaa jibu lake ni chakula na siyo kuangalia sinema na unapokuwa na hitaji la kuangalia sinema jibu lake sio chakula ni sinema. Hii haimaanishi chakula siyo kizuri ila siyo sahihi kwa hitaji.

Miongoni mwa wanandoa wengi suala la kwa nini wameoa au wameolewa linabaki ni ajenda ya siri hata kama bado wapo katika ndoa,na kipindi chote cha uchumba hawashirikishani majibu kwa maswali haya. Bahati mbaya kila mmoja anatarajia mwingine atafanya,inakuwa mbaya zaidi pale majibu yao yanapokuwa na radha tofauti yaani kama kutafuna karanga na dagaa kwa pamoja.

Na inawezekana kuna wengine wanaoana hata bila kuwa na haja ya majibu ya maswali haya lakini haimaanishi hawana ajenda zao. Kila nyuma ya tendo mwanadamu anafanya na hususani kubwa kama la ndoa zipo ajenda nyuma yake. Ujinga juu ya hili hauondoi ukweli wake.

Ilinichukua mwaka mzima kutaka kujua kwa nini nioe,sikutaka kuingia mahali kama giza. Nilitafuta kila mahali kujua na kwa uangalifu sana nilipaswa kumshirikisha mpenzi wangu. Baada ya muda mrefu nilipata jibu fupi sana ambalo nitakueleza kwa ufupi.... Sababu kubwa ni UPWEKE hii ni hamasa kubwa nyuma ya ke. Ilinipasa nirudi kuisoma mara kadhaa biblia yangu ili nijue ni kitu gani kilimsukuma Mungu amletee Eva kwa Adam na mara katika sentensi hii nikapata jibu. 

Wakati Adam alipokuwa akiwapa majina viumbe wengine wote ambao walipita mbele zake kwa jozi (pairs),lakini kwa Adam hakuonekana wa kufanana na yeye na hapa ndipo lilipozaliwa wazo la kumfanya Hawa kwa ajili yake. Na Upweke huu ni ule ambao hauwezi kukamilishwa na mzazi, ndugu au marafiki ndio maana sisi huamua kuwaacha hao wote ili tukaambatane na mmoja tu. 

Hitaji hili lipo katika kiini cha moyo wa mwanadamu na kama likishindwa kutimizwa ipasavyo haliwezi kuacha mahusiano yakawa salama...

Leo niishie hapa nitaendelea zaidi kesho kueleza kuhusu UPWEKE na athari zake katika mahusiano.

Nduguyo,
Ushindi Ellioth
Valentine gift box '17